|
Baadhi ya vijana waliojitokeza katika uwanja wa Taifa wa Nigeria uliopo Abuja wakiwa ndani ya uwanja huo baada ya kukanyagana |
Jumamosi ya Machi 15, 2014 kulitokea tukio la kusikitisha
katika nchi ya Nigeria ambapo angalau watu 16 walipoteza maisha katika harakati
za kutafuta kujikwamua kimaisha. Katika tukio hilo lililotokea kwenye mji wa Abuja,
dazani kadhaa za watu wengine walijeruhiwa vibaya.
Wanigeria hao walikutana na mkasa huo walipokua wakitafuta
kuingia ndani ya uwanja wa Taifa wa nchi hiyo ili kufanya mtihani ambao
ungewawezesha kupata fursa ya kufanya kazi katika Idara ya Uhamiaji ya nchi
hiyo. Uwanja huo una uwezo wa kuchukua watu 60,000 lakini Vyanzo vya habari
vinaeleza kuwa watu wasiopungua 68,000 walilipia N8000 kila mmoja kama gharama
ya kufanya mtihani huo. Idadi hiyo kubwa ya watu waliolipia kufanya mtihani
ilifanya idadi kubwa ya watu kufika katika Uwanja wa taifa wa Nigeria ili
kufanya mtihani huo.
Taarifa zinaeleza kuwa kulitokea kugombania kuingia uwanjani
humo ambapo watu walisukumana na kukanyagana. Watu wengine walijaribu hata
kuruka ukuta wa uwanja huo ili kuingia ndani. Hali hii ndio iliyopelekea mkasa
huo kutokea.
Mtihani huo ulikua ukiendelea pia katika miji mingine nchini Nigeria ya Lagos, Kaduna, Asaba na Benin.
Tunaweza kujiuliza ikiwa mamlaka husika zilijiandaa
kuhakikisha zoezi hilo linaenda kwa usalama, maana taarifa kutoka Abuja zinaeleza kuwa
kulikua na mlango mmoja tu wa kuingilia ndani ambao ulikua wazi. Hata hivyo
hili sio lengo letu hapa.
Tunachoshawishika kuamini ni kuwa jambo la msingi
lililopelekea idadi hiyo kubwa ya watu kujitokeza ni umaskini, au pengine ni
ukosefu wa ajira.
Hatujui idadi ya watu waliokua wanahitajika baada ya zoezi
hilo lakini tunaweza kujiuliza ikiwa watu zaidi ya elfu sitini walijitokeza
katika eneo hilo kwa wakati mmoja kuomba hizo kazi, tatizo la ukosefu wa ajira
ni kubwa kiasi gani?
Ukosefu wa ajira, za kuajiriwa au za kujiajiri,
kunasababisha umaskini. Umaskini huu ndio unaolirudisha bara letu la Afrika nyuma
katika kila nyanja.
Kwakua tunaamini kuwa mamlaka zinazohusika zinafahamu ukubwa
wa tatizo hili, na tatizo bado lipo, sisi swali letu la msingilinabaki kuwa,
tatizo la umaskini litaisha lini Afrika?