Acacia-land English Medium Pre and Primary School

Acacia-land English Medium Pre and Primary School
Acacia-land English Medium Pre and Primary School, P. O. Box 101, Igunga-Tabora. Phone: +255 784 545202

Monday, 17 March 2014

Tukio la Abuja: Tatizo la Umaskini litaisha lini Afrika?

Baadhi ya vijana waliojitokeza katika uwanja wa Taifa wa Nigeria uliopo Abuja wakiwa ndani ya uwanja huo baada ya kukanyagana

Jumamosi ya Machi 15, 2014 kulitokea tukio la kusikitisha katika nchi ya Nigeria ambapo angalau watu 16 walipoteza maisha katika harakati za kutafuta kujikwamua kimaisha. Katika tukio hilo lililotokea kwenye mji wa Abuja, dazani kadhaa za watu wengine walijeruhiwa vibaya.

Wanigeria hao walikutana na mkasa huo walipokua wakitafuta kuingia ndani ya uwanja wa Taifa wa nchi hiyo ili kufanya mtihani ambao ungewawezesha kupata fursa ya kufanya kazi katika Idara ya Uhamiaji ya nchi hiyo. Uwanja huo una uwezo wa kuchukua watu 60,000 lakini Vyanzo vya habari vinaeleza kuwa watu wasiopungua 68,000 walilipia N8000 kila mmoja kama gharama ya kufanya mtihani huo. Idadi hiyo kubwa ya watu waliolipia kufanya mtihani ilifanya idadi kubwa ya watu kufika katika Uwanja wa taifa wa Nigeria ili kufanya mtihani huo.

Taarifa zinaeleza kuwa kulitokea kugombania kuingia uwanjani humo ambapo watu walisukumana na kukanyagana. Watu wengine walijaribu hata kuruka ukuta wa uwanja huo ili kuingia ndani. Hali hii ndio iliyopelekea mkasa huo kutokea.

Mtihani huo ulikua ukiendelea pia katika miji mingine nchini Nigeria ya Lagos, Kaduna, Asaba na Benin.

Tunaweza kujiuliza ikiwa mamlaka husika zilijiandaa kuhakikisha zoezi hilo linaenda kwa usalama, maana taarifa kutoka Abuja zinaeleza kuwa kulikua na mlango mmoja tu wa kuingilia ndani ambao ulikua wazi. Hata hivyo hili sio lengo letu hapa.

Tunachoshawishika kuamini ni kuwa jambo la msingi lililopelekea idadi hiyo kubwa ya watu kujitokeza ni umaskini, au pengine ni ukosefu wa ajira.

Hatujui idadi ya watu waliokua wanahitajika baada ya zoezi hilo lakini tunaweza kujiuliza ikiwa watu zaidi ya elfu sitini walijitokeza katika eneo hilo kwa wakati mmoja kuomba hizo kazi, tatizo la ukosefu wa ajira ni kubwa kiasi gani?

Ukosefu wa ajira, za kuajiriwa au za kujiajiri, kunasababisha umaskini. Umaskini huu ndio unaolirudisha bara letu la Afrika nyuma katika kila nyanja.

Kwakua tunaamini kuwa mamlaka zinazohusika zinafahamu ukubwa wa tatizo hili, na tatizo bado lipo, sisi swali letu la msingilinabaki kuwa, tatizo la umaskini litaisha lini Afrika?




No comments:

Post a Comment