|
Jengo la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania |
Bunge la Bajeti linaanza leo mjini Dodoma huku
wabunge wakitarajiwa kuanza kulipwa viwango vipya vya posho, ambazo ni
Sh300,000 kwa siku sawa na kiwango wanacholipwa wajumbe wa Bunge Maalumu
la Katiba.
Kabla ya kufikia uamuzi wa kupandisha viwango
hivyo kwa Sh100,000 zaidi, wabunge walikuwa wakilipwa Sh200,000 kwa siku
(yaani Sh70,000 kama posho ya kikao (sitting allowance), Sh80,000 posho
ya kujikimu (perdiem) na Sh50,000 ya gharama za usafiri).
Nyongeza hiyo kwa kila mbunge kwa siku, sawa na
asilimia 50, italigharimu Bunge la Jamhuri ya Muungano kiasi cha Sh18.5
bilioni kwa siku 52 zilizotengwa kwa ajili ya Bunge la bajeti
linalotarajiwa kuhitimishwa Juni 27.
Januari mwaka 2012, Rais Jakaya Kikwete alikataa
maombi ya Bunge ya kutaka nyongeza ya posho ipande hadi Sh330,000 na
badala yake wabunge hao wakapata nyongeza ya Sh50,000 tu kwa ajili ya
usafiri.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililla alipoulizwa
kuhusu nyongeza hiyo, hakuthibitisha wala kukanusha, lakini akafafanua
kwamba hilo ni suala la uongozi wa Bunge na si la kiutendaji.
“Suala la malipo kuongezeka au kutoongezeka
kimsingi siyo kazi ya Ofisi ya Katibu wa Bunge, vipo vyombo vya juu vya
uongozi wa Bunge; Kamati ya Uongozi na Tume ya Huduma za Bunge, na
vyombo vyote vinaongozwa na Spika. Kwa hiyo, kama kuna nyongeza, sisi
tunapewa taarifa tu kwa ajili ya kutekeleza,” alisema Dk Kashililla na
kuongeza:
“Hadi sasa sina taarifa rasmi kuhusu suala hilo,
ikiwa litafika mezani kwangu kama maelekezo, tutatekeleza kwa mujibu wa
maelekezo husika.”
Habari ambazo zimelifikia gazeti hili kutoka
vyanzo mbalimbali ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
zinasema, uongozi wa muhimili huo umeamua kuanza kulipa kiasi hicho cha
fedha kutokana na shinikizo kubwa kutoka kwa wabunge.
Taarifa za kuwapo kwa msukumo wa ajenda ya
kupandisha posho za wabunge zilianza kusikika wakati Bunge la Katiba
likielekea ukingoni, wakati wabunge walikuwa wakihoji sababu za wajumbe
kulipwa kiasi kikubwa cha fedha kwa kazi ileile na katika mazingira
yaleyale, wakati wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wakilipwa kiasi
kidogo.
“Msingi wa hoja yetu hapa ni kwamba maisha na
mazingira ya Dodoma ni yale sasa, leo kwanini wajumbe wa Bunge la Katiba
walipwe Sh300,000 sisi tulipwe kidogo kuliko hicho?” alihoji mmoja wa
wabunge.
“Na usisahau mwanzoni tu pale (mbunge wa Sumve,
Richard) Ndassa alitoa hoja akisema posho hiyo ya Sh300,000 haitoshi kwa
kuwa gharama za maisha Dodoma zimepanda... Gharama haziwezi kupanda
Bunge la Katiba pekee.”
Mbunge huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake,
alisema kama kigezo ni gharama za maisha, mazingira hayo ndiyo
wanayokutana nayo wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Spika wa Bunge, Anne Makinda licha ya kutafutwa mara kadhaa
hakupatikana kuzungumzia suala hilo, lakini Naibu Spika wa Bunge, Job
Ndugai alikiri kuwapo kwa msukumo wa wanaotaka nyongeza ya posho, lakini
akasema suala hilo halijafanyiwa uamuzi.
“Hata mimi nimesikia kama ulivyosikia wewe. Ni
suala ambalo wabunge wamekuwa wakilizungumza, lakini uamuzi ni mchakato
si suala la mtu mmoja. Ninavyofahamu mimi uamuzi ulikuwa haujafanyika,”
alisema Ndugai.
Awali kulikuwa na taarifa kwamba maombi ya
nyongeza ya posho yamepelekwa kwa Rais Kikwete kwa ajili ya kupata
idhini yake, lakini Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema
hakukuwa na maombi ya aina hiyo. “Kusema kweli maombi hayo sijayaona. Kama yakija
tutayashughulikia kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo maana ukweli
ni kwamba nyongeza zinategemea uwezo wa Serikali kulipa kwa maana ya
bajeti kama ipo,” alisema Sefue.
Hata hivyo, gazeti hili limethibitishiwa kuwa
uongozi wa Bunge umelazimika kubana sehemu ya matumizi yake katika
maeneo mengine hivyo kuwezesha kupatikana kwa kiasi cha fedha
kinachotakiwa kwa ajili ya nyongeza wakati wa Bunge la Bajeti.
“Bunge lina bajeti yake kwa hiyo walichofanya ni
kupunguza matumizi katika sehemu nyingine kama vile safari na hilo
limefanyika, hivyo uwezo wa kulipa kiasi hicho kinachotakiwa upo,”
alisema mpashaji wetu kutoka ndani ya Ofisi za Bunge na kuongeza:
“Hilo linafanyika kwa kipindi hiki cha Bunge la
Bajeti, baada ya hapo nyongeza hiyo itazingatiwa katika mapendekezo ya
bajeti ya 2014/15”.
Mmoja wa maofisa wa Bunge aliliambia gazeti hili
kwamba hakukuwa na njia ya uongozi wa taasisi hiyo kukataa kulipa fedha
hizo kutokana na ukweli kwamba wangepata wakati mgumu kutoa maelezo kwa
wabunge.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi licha ya kukiri kuwapo kwa madai ya
wabunge kutaka nyongeza ya posho, naye hakuwa tayari kulizungumzia kwa
undani kwa maelezo kwamba yeye hakuwapo nchini kwa muda mrefu.
“Mimi kwa kweli nisamehe tu ndugu yangu. Sikuwapo
nchini kwa muda maana nilikwenda nje kwa ajili ya masuala ya afya, hivyo
sijapata muda wa kufahamu kilichozungumzwa na kukubaliwa kuhusu suala
hilo,” alisema Lukuvi.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi