Niliwahi kupata bahati ya kusafiri kwa basi kati ya
Lilongwe, Malawi na Dar es Salaam, Tanzania. Ilituchukua jumla ya masaa 30 kusafiri kutoka Lilongwe hadi Dar. Kimsingi ilikua ndio safari yangu ya kwanza ndefu
kiasi hicho kusafiri kwa basi.
Safari ilianzia Devil Street, Lilongwe saa moja kamili jioni (kwa saa za Malawi, sawa na saa mbili usiku kwa saa za Tanzania) kwa basi la kampuni ya TAQWA. Kilichonifurahisha wakati wa kuanza safari ni imani waliyonayo Wamalawi kwa Mungu kwani safari yetu ilianza kwa sala. In fact, nimewahi kupata fursa ya kuhudhuria mikutano na vikao kadhaa vya kiofisi nchini Malawi, tena ni vya kiserikali, ambapo asilimia kubwa ya vikao hivyo vilikuwa vikifunguliwa kwa sala! Nchini kwetu vikao vinavyofunguliwa kwa sala labda ni vya taasisi za kidini.
Basi la kampuni ya TAQWA tulilosafiri nalo |
Kitu nilichogundua haraka haraka ni kuwa wengi wa abiria waliokua kwenye TAQWA walikua wafanyabiashara. Wanachukua mzigo Dar (hasahasa kariakoo) wanapeleka Malawi. Walikuwemo wafanyabiashara wa kitanzania na kimalawi. Nikagundua kumbe raia wa nchi hizi mbili wana uhusiano mzuri wa kibiashara.
Kituo cha kwanza kusimama kilikua katika hoteli ya Seven Eleven iliyopo katika jiji la Lilongwe. Pale tulisimama kwa ajili ya kununua chakula. Ni ruhusa kwa magari ya abiria kusafiri usiku katika nchi ya Malawi, kwa maana nyingine safari ni masaa 24.
Baada ya abiria kujinunulia vyakula vyao kwa ajili ya usiku ule, safari ilianza tena kwenye saa mbili kasorobo hivi za Malawi. Tulifika Mzuzu kwenye saa saba za usiku ambapo basi lilisimama kupakia abiria wengine waliokua wakielekea Tanzania.Nakumbuka kabla ya kufika Mzuzu tulisimamishwa njiani na askari kama mara mbili tu.
Baada ya Mzuzu hali ilibadilika. Ilikua ni mwendo wa kukutana na mageti ya askari wa uhamiaji. Kuna mahali tulisimamishwa, usiku huo, tukaamrishwa wote tushuke chini ili wakague hati zetu za kusafiria (Passport). Ilikua ni usiku sana, halafu ni porini na mahali pale palikua na baridi kali sana. Abiria waliwaomba askari hao waingie kukagua hizo hati ndani ya gari kwa maelezo kuwa nje hapakuwa na usalama wa kutosha na pia kulikua na baridi sana.
Askari walivosikia vile wakamuamrisha dereva kuzima gari, na kutueleza kuwa kama hamtaki kushuka mtalala hapahapa. Abiria walijaribu kuweka mgomo wa kushuka lakini askari hawakuwaelewa. Baada ya dakika kama 15 hivi tuliamua kushuka huku abiria wakiwatolea wale askari maneno makali. Kuna mama mmoja, mmalawi, alisikika akisema (kwa Kichewa), "nyie askari wa Malawi mnapenda sana kuabudiwa, nendeni Tanzania mkajifunze kwa wenzenu... sisi sio wahamiaji haramu, ni Wamalawi wenzenu kwanini mnatutesa na baridi hivi usiku huu..?". Mwanaume mwingine mtanzania yeye ndio kidogo alete tafrani. Aliwaambia wale askari kwa Kiswahili (sijui alikua anafikiri hawajui Kiswahili au aliamua tu kusema ili liwalo na liwe), "...mnashindwa kulala makwenu mnakuja kukesha huku porini... nchi yenyewe maskini, haina tembo, haina almasi, haina dhahabu, haina rasilimali zozote... mtu atakuja kuzamia huku kutafuta nini... wenzenu wanatafuta kuungana nyie mnatafuta kujitenga!..." Kuna askari mmoja alikua juu ya gari (Pick up) akayasikia yale maneno, aliruka chini kama mshale kuja kumkamata yule bwana, ila abiria kwa umoja wao walimzingira yule askari wakimzuia asimkamate. Mwishowe askari akaona isiwe taabu akaachana nae.
Zoezi la ukaguzi wa Passport lilikua la abiria mmoja baada ya mwingine, ukishakaguliwa ndio unaruhusiwa kuingia ndani ya gari. Baada ya hilo zoezi safari iliendelea, ila kama kawaida mageti ya ukaguzi yalikua mengi japo hatukuwahi tena kushushwa chini. Safari iliendelea mpaka tulipofika Songwe, mpakani mwa Malawi na Tanzania kwenye saa kumi na mbili kasorobo hivi alfajiri kwa masaa ya Tanzania.
Geti la mpakani upande wa Malawi likiwa bado limefungwa, asubuhi hiyo |
Basi tulilokuwa tukisafiri nalo likisubiri geti la mpakani lifunguliwe |
Magari mengine yakiwa mpakani upande wa Malawi yakisubiri geti la mpaka lifunguliwe |
No comments:
Post a Comment